Thursday, June 7, 2012

Riwaya mpya ya Kiswahili

UTANDAWAZI AU UTANDAWIZI? JINSI LUGHA YA RIWAYA MPYA YA KISWAHILI INAVYODAI Said A.M. Khamis 1.0 Utangulizi Kuzuka kwa riwaya mpya ya Kiswahili katika miaka ya 1990 kunaelezwa kwa viwango mbalimbali na wahakiki kama vile Wamitila (1991, 1997), Gromov (1998, 2004), Khamis (1999, 2001, 2003, 2004), Bertoncini (2002), Topan (2002), King’ei (2002), Dittemer (2002/2003) na Rettová (2004). Hapa, hatuna nafasi ya kurejelea tabia za ‘kimaumbo’, ‘kimiundo’ na ‘kimaudhui’ zinazoitofautisha riwaya hii ya Kiswahili na nyingine, ila tutajishughulisha na kipengele kimoja tu cha msingi, nacho ni kipengele cha lugha kama alama mojawapo ya mtindo1 au mwelekeo wa riwaya hii – lugha katika uhusiano wake na utandawazi au utandawizi. Katika makala haya tunatilia mkazo kwamba aina ya lugha inayotumika katika kazi fulani ya fasihi huathiriwa na nini kinachotokea katika jamii yenyewe ambamo mwandishi huchota fikira, maudhui, falsafa, itikadi, jazanda, mitindo, maumbo na miundo-lugha –hasa inapokuwa jamii yenyewe imo katika kasi ya mabadiliko makubwa kama ambavyo tumekuwa tukishuhudia kuanzia wakati riwaya hii ilipoibuka katika miaka ya 1990 hadi leo. 2.0 Riwaya Mpya na Utandawazi Riwaya ya Kiswahili tunayoizungumzia imezaliwa mwanzoni mwa miaka ya 1990, muda mfupi tu baada ya neno utandawazi kuingia masikioni na kuzama akilini mwetu kuanzia miaka 1980. Utandawazi ni neno dhahania mno, lenye maana nyingi zenye utata kutegemea msisitizo wa anayelitumia. Pamoja na tofauti za maana na matumizi ya neno hili, wataalamu wanakubaliana kwamba ni neno linaloelezea mfungamano na uhusiano uliojitokeza katika miaka 30 iliyopita; hasa katika biashara na uchumi, lakini pia katika utamaduni, miongoni mwa jamii tofauti za dunia. Mfungamano na uhusianao huu unatofautishwa na mfungamano na mahusiano mengine ya aina hii yaliyojitokeza hapo awali, kwa sababu utandawazi umepata kasi kubwa ya kuwekeza mitaji na kuvuna bamvua la faida kiuchumi na kiutamaduni; ukisaidiwa na maendeleo makubwa ya kiteknolojia yaliyopatikana karibuni, hasa ya vyombo vya mawasiliano ambavyo vimefupisha au kuondoa vikwazo vya masafa na wakati (Jauch 2001, Offiong 2001). Kiutamaduni, utandawazi unahusishwa na kuenea kwa tamaduni za ki-Magharibi kwa njia ya kibiashara (k.m vinywaji vya Coca Cola, bia na pombe kali ambazo hapo zamani zilikuwa hazijulikani au zilijulikana kwa watu wachache tu wa Dunia ya Tatu na vyakula vya Kentucky na Mcdonald) au mtiririko wa muziki na taswira kupitia video, televisheni, mitandao ya kompyuta na simu, CD, DVD na VCD. Lakini kwa hakika si sahihi kuuchukulia utandawazi kijuujuu tu, au jinsi unavyofasiliwa na watetezi wake. Kwa hivyo, ipo haja hapa kuelezea, ingawa kwa ufupi, asili ya kuibuka kwake. Historia ya utandawazi haiwezi kuepushwa na misingi ya mikakati ya G7, Benki ya Dunia, IMF na WTO, vyombo vinavyosimamiwa, kuimarishwa na kuendelezwa na itikadi ya uliberali-mpya2 (Jauch 2001; 3-15; Offiong, 2001: 1-19). Kwa kweli, 1 Tunapenda kukumbusha kwamba hii ni maana moja tu ya mtindo – yaani mbinu ya pamoja inayotofautisha kundi la 2 Tafsiri ya ’neo-liberalism’ kinadharia, mfungamano na uhusiano huu wa utandawazi unafasiliwa kwa namna tofauti baina ya kambi mbili. Kambi ya kwanza inauchukulia utandawazi kuwa ni ‘baraka’ kwa nchi zote duniani, kwa sababu hatimaye utaboresha maisha ya watu wote duniani kote (Ruigrok & Van Tulder 1995:169). Kambi hii inadai kwamba utandawazi una faida kubwa hasa kwa nchi zinazoendelea3, na kwamba kufungua milango ya biashara, masoko huria ya bidhaa na kuufanya utamaduni wa taifa moja ukutane uso kwa uso na utamaduni wa mataifa mengine (sifa moja kubwa ya utandawazi), kunaleta fanaka kila pahala (Jauch, keshatajwa: 3). Kambi ya pili, ikitumia ithibati jarabati, inakanusha kabisa uhalali wa madai ya kambi ya kwanza, kwa kusema kwamba utandawazi si dhana mpya kamwe, bali ni upeo wa dhana kongwe yenye sifa mpya ya kutumia maendeleo makubwa yaliyopatikana kiteknolojia, kunyonya, kwa mapana na marefu, utajiri wa dunia na kuwaacha watu wa nchi masikini kuwa masikini zaidi kuliko walivyokuwa zamani. Na si kuwaacha masikini zaidi tu, bali pia kuchafua uchumi, tamaduni, mazingira na maisha yao vibayavibaya, hadi kufikia nchi hizo kudharauliwa na kuonekana si lolote si chochote katika fikra ya dunia hivi leo. Mabadiliko haya, kwa sehemu kubwa, yanatokana na upeo wa matatizo ya kiuchumi ya kimataifa yaliyotokea mwanzoni mwa miaka ya 1970, ambayo yalisababishwa na maslahi ya kibiashara na utashi wa mataifa makubwa yanayolenga kila siku kupata faida kubwa kupita kiasi (Murray 2000:7-8; ILRIG 1998). Jumla ya riwaya za Kiswahili tunazoita mpya ni zile za Euphrase Kezilahabi za Nagona (1990) na Mzingile (1990), riwaya moja ya Katama Mkangi ya Walenisi (1995), riwaya ya W. E. Mkufya ya Ziraili na Zirani (1999), riwaya moja ya Mohamed ya Babu Alipofufuka (2001) na miswada yake miwili4 ya Dunia Yao na Mkamandume, riwaya moja ya Wamitila ya Bina-Adamu (2002) na, kwa namna na kiwango fulani, riwaya ya Chachage ya Makuadi wa Soko Huria (2002). Sifa moja kubwa ya kimaudhui, miongoni mwa sifa kadha za riwaya hii, ni ile ya kushughulikia kwa kina matatizo ambayo yanaukabili ulimwengu wetu leo. Kwa namna nyingine tunaweza kusema, ingawa bado riwaya hii inajishughulisha kwa kiwango fulani, na matatizo ya ndani ya nchi na jamii husika, kwa kiasi kikubwa imekiuka mipaka ya kitaifa na kieneo. Kwenye jalada la nyuma la Bina-Adamu, tunaambiwa wazi kwamba… [n]i riwaya inayotumia sitiari ya kijiji kuangalia hali ya mataifa ya ulimwengu. Katika kuhitimisha makala yake Postmodernistic Elements in Recent Kiswahili Novels, Gromov (2004:13) anatuambia: [t]unaweza kusema kwamba fasihi ya Kiswahili inaendelea kuchukua dhima ya uchunguzi wa jamii –lakini, huku ikibeba silaha mpya za njia ya utunzi na fikra za majadiliano, inajishughulisha na matatizo mapya, na inachunguza, si jamii ya Afrika Mashariki tu, bali dunia yote kubwa (na) pumbavu, isiyoishika tena, lakini ndiyo pekee tuliyonayo– dunia yetu ya leo ... (tafsiri yangu). 3 Sina hakika kwamba neno hili tunaweza kuendelea kulitumia kurejelea nchi zetu za Kiafrika, lakini nitalitumia kwa kukosa neno linalofaa zaidi. 4 Dunia Yao ni mswada uliopelekwa Jomo Kenyatta Foundation tangu 2001 na kukubaliwa kuchapishwa lakini mwandishi aliuondoa huko, kwa kuchelewa kuchapishwa, akaupeleka OUP ambako nako umekaa tangu Julai, 2004. Ms wa Mkamandume ulimalizwa kuandikwa mwaka 2004 na bado haujawasilishwa kwa watoa vitabu wowote. Ingawa riwaya hii mpya, kama tulivyosema, inajishughulisha na mada mbalimbali za kimaudhui kuhusu matatizo yanayoikabili dunia yetu ya leo –hapa tumechagua kuzungumzia, kwa mujibu wa maoni yetu, tatizo kubwa na sugu kabisa la utandawazi– tatizo ambalo riwaya kama Nagona, Mzingile, Babu Alipofufuka, Dunia Yao, Bina- Adamu na Mkamandume, zinalijadili waziwazi. Kwa mfano, katika kuthibitisha namna gani dhamira ya utandawazi inavyotawala katika Bina-Adamu, Gromov (2004:8), akiteua kwa uangalifu lugha na picha zinazoelezea dhana ya utandawazi, anatambia hivi: Wakati wa safari yake ndefu, mbabe, akisaidiwa na sauti ya ajabu ya mwanamke mwenye sifa zisizo za kibinamu anayeitwa Hanna, anazuru Ulaya ambayo ‘inaishi jana’, Asia ya viwanda ambayo ‘inaishi kwa matumaini’ na Afrika, ambayo ‘inaishi mwishoni mwa kijiji cha utandawazi na imeharibiwaharibiwa na njaa na vita. Anapokuwa njiani, kila pahala anakutana na mambo yanayoonekana hayana mantiki, mambo ambayo hayaelezeki yanayofanywa na P. P mwenye miujiza –Ulaya P. P ameushinda ufashisti, lakini bado unaishi imara miongoni mwa wafuasi wake. Huko Asia ametupa bomu la Atomiki Hiroshima. Afrika, akitumia jiwe, amevigonga vichwa vya wanasiasa kuvitoa akili. Huko Urusi, ambako P. P anazuru kwa muda mfupi, hatuambii anafanya nini kwa vile anamwogopa Stalin. P. P anaiuza Afrika kwa watalii wa kigeni, anaharibu bahari kwa mafuta na mabaki machafu ya ‘radioactive’: Mwishoni mwa safari yake mbabe anaigundua Amerika –Bustani ya Adeni ya pili, ambamo wakazi wake, mapapa wa biashara za kimataifa, wanaishi (vizuri) kutokana na umasikini wa Nchi za Dunia ya Tatu, wakidai kwamba wanaishi leo na tena wanaishi katika uhalisia wa mambo ... (tafsiri yangu) Msomaji anaposoma lugha hii, anaona moja kwa moja kwamba huu ni mfano mmoja wa waandishi wa riwaya hii ambao wanapinga kwamba utandwazi una neema yoyote ile kwa nchi za Dunia ya Tatu. Na kusema kweli, hawaishii hapo tu. Wanaonyesha hasira zao kwa kile ambacho wao wanaona ni ujinga wa viongozi au serikali zetu kukubali kiholela kuihonga nchi kwa mataifa makubwa. Itakuwaje mataifa G7 ambayo yalitukandamiza kwa kila hali wakati wa ukoloni ndio leo yawe yanayotutakia mema? Itakuwaje vyombo kama Benki ya Dunia, IMF na WTO ambavyo vimekuwa vikitoa mikopo kwa masharti magumu mpaka kutunyang’anya uhuru wa kila kitu, viwe ni vyombo vya kutufikisha pahala pema? Itakuwaje itikadi ya uliberali-mpya iwe ndiyo itikadi ya kusafiria kwa nchi za kimasikini? Itakuwaje nchi zetu ziweze kuingia katika mashindano ya kibiashara na USA, Ulaya ya Magharibi, Japani, Australia na Korea ya Kusini? Vipi suala la ndizi za Jamaika? Je, huu haukuwa mfano wa kutosha wa kutufumbua macho? Wakulima wetu wanawezaje kushindana katika uzalishaji na uuzaji wa bidhaa na wakulima wa mataifa makubwa yanayopata fidia kubwa kutoka serikali zao? Hivi historia nzima ya udhalimu wa ukoloni na ukoloni mamboleo, haijawa funzo la kutufanya tushituke na kuuangalia uhusiano wetu na dunia upya na kwa makini zaidi? Kwa mujibu wa waandishi wa riwaya hizi, kukubali kudanganyika kirahisi na mambo haya, kumesababisha kuporomoka vibaya sana kwa nchi zetu katika sekta zake zote, ingawa takwimu za ukuaji wa uchumi zinazotolewa na wakubwa, zinawekwa juu. Hii ndiyo sababu mwandishi mmoja kati yao, Wamitila (keshatajwa: 85, 87, 155), ametumia neno utandawizi, badala ya utandawazi – kijiji cha Global Villain, global pillage. 3.0 Matumizi ya Lugha katika Riwaya Mpya Kwa ujumla, lugha ya aina hii ya riwaya mpya ya Kiswahili ina tabia tofauti na lugha ya aina nyingine za riwaya ya Kiswahili tangulizi ambazo zimekita kwenye uhalisia mkavu. Sifa ya mwanzo na ambayo ni ya msingi, ni ile ya usasabaadaye, ambao, kama mtindo fulani wa fasihi na sanaa kwa ujumla, unakwenda sambamba na utandawazi au ubepari mpevu, kuonyesha mkinzano mkubwa uliomo ndani ya mfumo wake. Usasabaadaye ni mfumo ambao huvunja kanuni zote za kijadi, kaida na namna ya kutumia lugha kisanaa. Sifa ya pili ni ya utouzowefu5 neno lililoanzishwa na shule ya urasimukanuni lenye kubeba maana na kazi maalumu katika fasihi –kazi ya kuichangamsha na kuitia lugha uvuguvugu ili inonekane mpya au ngeni kuliko ilivyokuwa, lengo kubwa likiwa kubadilisha mtazamo wa msomaji kwa kumwonesha ujumi wa lugha ambao utachukua makini ya msomaji, kumvuta kisanaa na kumfanya afikiri zaidi. Kwa mfano Mohamed katika Babu Alipofufuka (2001:13) anacheza na lugha kwa namna ifuatayo: [I]nasemakana Delpiero karibuni amemeza eneo zima la ardhi la pahala fulani tumboni mwake. Wavuvi waliposimama kidete kupuliza cheche zao za uchungu, K alikuja juu kuwaambia wastarehee neema zao ... Sifa ya tatu ambayo pia inashikana na sifa ya mwanzo na ya pili ni ile ya mvutogubi6. Neno hili linasimamia mjazo wa jazanda zenye fumbo, nguvu na mapigo ya kimuziki ambayo mara kadha huonekana ni muhimu zaidi kuliko maana – ingawa katika riwaya hii maana bado inabaki kuimarishwa. Hapa kwa mfano, tuna mchezo wa mvutogubi kutokana na riwaya ya Wamitila, Bina-Adamu (2002: 40): [S]ikujua kama nilikuwa nikitembea kuelekea jana au kwenda kesho au labda nilikuwa leo. Labda nilikuwa kote wakati mmoja ... Sifa ya nne, ni ile ya mchanganyo ndimi, hasa kwa sababu riwaya hii mara nyingi husomba na kujaza kila kitu katika matini yake: historia (‘Vita vya Fyura’ – Bina-Adamu uk. 34), uchumi (‘Nchi nyingi katika ulimwengu wa tatu zilipata pigo kubwa la njaa na mamilioni ya watu walikufa. Migogoro mingi ya kiuchumi iliendelea kuisakama dunia’ – Nagona uk. 18), siasa (‘Dunia yao ndivyo ilivyo; si hii yetu: Kwao taka husafishwa kwa taka; uungwana husafishwa na utumwa –madhali tu K anaramba kamasi tamu za pua...’ – Babu Alipofufuka uk. 10), utamaduni (‘Tupige darubini hivi vitu tunavyovikimbilia kutoka nje. Hizi video na filamu ni propaganda isiyokuwa ya moja kwa moja. Zinatumiwa kusambaza na kutangaza taswira maalumu za utamaduni mmoja tu...’ Bina- Adamu uk. 40), muziki (‘Nilipoingia ndani nilitia CD ya wimbo wa taarab wa Mohamed Ilyas: La Hasha!’ –Dunia Yao uk.87). Kisaikolojia, riwaya zote zinaonyeshwa akili za wananchi kufunikwa na utandu. Kwa matatizo ya utandawazi na mengine yanayoibua matatizo ya kisaikolojia na kisosholojia, mkondo mzima unaomchukua mwanadamu kubadilika na kuwa mnyama, unachunguzwa katika riwaya hizi kupitia kile ambacho tungeliweza kukiita sosiolojia ya riwaya. Aidha mna mchanganyiko wa visaasili, migani na harafa. 5 Tasiri ya Defamiliarisation ambayo ni tafsiri ya ’ostranenie’, neno la Kirusi lililoanzishwa na Viktor Shklovsky 6 Tafsiri ya Hermetic 3.1 Lugha na Usasabaadaye Kwa vyovyote vile, chochote kile kinachohusiana na kilichomo ndani ya fasihi na jinsi kinavyowasilishwa katika kazi hiyo, lazima kihusishwe na matumizi mbalimbali ya lugha. Makala haya yanatambua ukweli kwamba kile ambacho, kwa mfano, kinaitenga lugha ya sayansi na fasihi ni jinsi lugha inavyojitokeza tofauti kimaumbo, kimsamiati na kimuundo katika nyanja hizi mbili. Ukweli huu umo pia katika namna lugha za ushairi na nathari, uhalisia na fantasia, usasa ulioanza baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia; na usasabaadaye, ulioanza baada ya Vita vya Pili ya Dunia na kwenda mbele zaidi kuigeuza riwaya ya uhalisia jinsi ilivyokuwa kabla ya kuzuka kwa usasa huko Ulaya. Usasabaadaye, kama njia moja ya kubuni kazi za fasihi, ulianza mapema tokea miaka 1950, baada ya kuporomoka kwa uhalisia na usasa. Lakini ni katika miaka ya 1980 ndipo usasabaadaye ulipopata upana wa matumizi katika nyanja za falsafa na utamaduni na pia katika fasihi na uhakiki wa kifasihi (Gromov 2004:1). Lengo kuu la usasabaadaye, kinyume na uhalisia na usasa, ni kuonyesha kutoweza kwa mwanadamu kuufahamu ulimwengu, kwa sababu urazini wa mwanadamu hauwezi tena, katika hatua hii, kuutambua utata wa ulimwengu. Kile kinachowezekana labda ni kuchunguza picha au alama za vitu. Hii ni kusema kwamba mwanadamu haufahamu ulimwengu wake kwa sababu tu umekuwa ni ‘uwanja wa fujo’, bali pia kwa sababu ni kama matini tu; yaani mlimbikizo usiokuwa na mwisho wa alama zinazobuniwa kutokana na urazini wa mwanadamu. Kwa hivyo, uzoefu wa mwanadamu, historia yake, utamaduni wake –kila kitu ni mkondo wa alama, ambamo zile zilizo tata hutokana na zile sahili zilizokuwepo hapo awali. Hapa tutaitazama lugha ya riwaya mpya katika ugo huo. Lakini kabla hatujafanya hivyo, yafaa tukawazindua wasomaji wetu juu ya jambo moja ambalo Gromov (keshatajwa) analieleza na ambalo ni la kipekee katika riwaya hii mpya ukilinganisha na usasabaadaye katika fasihi za lugha na tamaduni nyingine. Jambo hili linahusiana na namna waandishi wa riwaya hii mpya wanavyobaki kung’ang’ania tamaa na kutukuza utu na ubinadamu. Katika hitimisho lake Gromov (keshatajwa: 12-13) anatwambia ... [l]azima tugundue kwamba kuna tofauti kubwa baina ya umahiri wa usasabaadaye wa nchi za ki-Magharaibi na ule wa jamaa zao wa Afrika Mashariki, Kiswahili kinakozungumzwa. Waandishi wa Kiswahili katika kuvutika na usasabaadaye wana mtazamo na msimamo wa pekee kuhusu maana na umuhimu wa ujumi ukilinganisha na ule wa wanausasabaadaye wa ki-Magharibi –wanausasabaadaye wa Kiswahili wana mtazamo mkali juu ya kuvunjiwa thamani dunia. Katika mtazamo wao mkali, waandishi wa riwaya mpya ya Kiswahili, utu na mapenzi vinatetewa kama tunavyosoma katika Bina-Adamu, pale mhusika mkuu Binadamu Msafiri anapoonywa kuutunza mkoba aliopewa na babu na kuambiwa ... [U]tunze huu, ndani mna utu, mapenzi na kiini cha kuwako kwako. Mkoba huu utakufaa sana siku zijazo: Usiudharau kwa sura yake; mwacha asili ni mtumwa ... Makala haya yanakubaliana sana na Gromov kuhusiana na ugunduzi huu muhimu wa suala la utu na mapenzi katika riwaya mpya ya Kiswahili na waandishi wake. Lengo mojawapo la makala haya ni kudhihirisha hivyo. 3.2 Lugha ya Uhakiki na Mkemeo wa Utandawazi Waandishi wa riwaya mpya ya Kiswahili katika uhakiki wao wa siasa na mwenendo wa jamii, wanataja wazi kwamba umefika wakati sasa Mwafrika ajilaumu mwenyewe juu ya balaa lote linalomkuta; na la kulaumiwa zaidi, hasa, ni taratibu za uongozi zitumikazo katika Afrika. Kuhusu suala hili Mohamed, katika Babu Alipofufuka (uk.10) anatuambia: [S]iku hizi K, kinyinginya changu, anaweza kuketi meza moja na watu ambao miaka michache iliyopita ilikuwa mwiko kukaa nao. Mazimwi, aliwaita. Akatangaza vita nao kwa kusaidiwa na nyuki... Kwa waandishi hawa, kuwakaribisha mabeberu, bila au kwa viwango vilivyopo vya malipo ya uwekezaji ili kuchukua rasilimali za nchi zetu na kutumia jasho la watu wetu, ni ujinga usiokuwa na mfano. Mohamed katika Babu Alipofufuka (uk.13-14) akiwaelezea wahusika wake wa kigeni anathibitisha tena ujinga huu kwa maneno haya: [I]nasemekana Delpiero karibuni amemeza eneo zima la ardhi la pahala fulani tumboni mwake. Wavuvi waliposimama kidete kupuliza cheche zao za uchungu, K alikuja juu kuwaambia wastarehee neema zao... Miyazawa aliyetoka kwao juzijuzi na kuwa mwenyeji kuliko wenyeji, haonekani na mtu yeyote kuwa na kazi ya maana nchini humo ila sifa zake za mkonowazi... Naye Von Heim, ana nia kubwa ya kusaidia kumfufua maiti kwa kummiminia bia kutokana na tangi lake kubwa... Tena kulikuwa na Di Livio ambaye kaja huku kucheza kamari. Halali mchana wala usiku; yumo mbioni vilabuni, mabasini, mandarini, hotelini... Kusema kweli, ujinga wetu hauko katika kukubali kuibiwa tu rasilimali zetu, bali pia kukubali kupokea vibovu na vichafu kwa thamani kubwa. Wamitila (keshatajwa) anaiendeleza fikra hii kwa maneno haya: “Hiki ni kiwanda.” “Cha nini?” “Reconditioned cars.” “Mnazitumia?” “Ahh, deki masen! Haiwezekani asilani. Sheria zetu zinakataza matumizi ya magari hayo.” “Basi mnayetengenezea nini?” “Kuna soko kubwa huko upande wa chini. Huko ndiko tunakotupa tusivyovihitaji.” “Mnavitupa ehh?” “Mmm, ni hivi tuseme, wanakubali wenyewe; ...” Kauli kali kabisa ya uhakiki na mkemeo wa waandishi hawa kuhusu ujinga wetu unapatikana katika mswada wa riwaya ya Mohamed, Dunia Yao (38), kauli ambayo inathibitisha jinsi gani tulivyotoa nafasi kutawaliwa, kwa kuogopa kutopata ruzuku au kwa kutarajia uokovu kutokana na utandawazi: Wamechukua kila kitu: niliendelea; wao wamekuwa ndio wafikiri wetu, wasemaji wetu, wanaohisi kwa ajili yetu, wanaoona njaa na kiu zetu, walimu, madakitari, wanafalsafa, wanauchumi, mashehe, mapadre, walinzi wetu ... kwa ujumla waendesha maisha yetu yote; sehemu ya viwiliwili na akili zetu ... kwa ufupi wao ni kila kitu! Sisi wengine ni mapipa matupu. Hatuna rojo la uhai: Hatuna supu ya maisha wala nyama ya ubinadamu wetu. Hatuna sehemu ya utu. Hatuna rai. Hatuna maoni. Hatuna chetu. Hatuwezi kufikiri kama wao au zaidi ya wao. Hatutarajiwi kusema. Hatutarajiwi kushiriki hata mambo yanayohusu nafsi zetu. Chambilecho Fowles... Kuna mtazamo fulani wa kisasa katika dunia yetu kwamba falsafa waachiwe wanafalsafa, elimujamii iwe bahari ya kuogelewa na wanaelimujamii na kifo kwa maiti. Lugha hii ya uhakiki na mkemeo kwa utandawazi inakita katika kauli, picha na jazanda zinazojenga kejeli au tashititi. Katika matumizi ya lugha ya namna hii waandishi hawa wanatoa dalili ya ujinga wa jamii na uongozi wao na uchungu walionao kwa ujinga huo unaotendeka –dalili ambazo zinaweza kupewa tafsiri tofauti miongoni mwa wasomaji. Kwa mfano, haifahamiki nani kaelekezwa nalo dondoo hilo hapo juu: utawala wetu wa ndani? Makuadi wa soko huria? Ukoloni mamboleo? Wakoloni mamboleo wenyewe? Utandawazi au waasisi wa utandawazi na vyombo vyao? Utandawizi ambao unajidhihirisha katika mshuko wa kiwango cha chini kabisa katika heshima ya dunia? Uelezaji huu unalingana na unakwenda sanjari na utata na mkinzano wa mambo mengi jinsi yanavyokwenda katika dunia yetu ya leo. Fikiria utata na mkinzano wa utawala au uongozi wetu wa ndani na haki za raia zinazovunjwa ovyoovyo. Fikiria ukoloni mamboleo na utandawazi wenyewe unavyovunjavunja kila kitu na jinsi matokeo yake yanavyoafikiana sana na matumizi ya lugha katika riwaya hii. 3.3. Ujengaji Fantasia na Uhalisia Mazingaombwe Sifa iliyo dhahiri sana katika riwaya hii ni namna gani lugha inavyotumiwa kujenga kwa makusudi fantasia na uhalisia mazingaombwe. Katika makala haya tunatofautisha fantasia na uhalisia kwa sababu fantasia ni dhana inayoelezea njia ya kutumia lugha kwa kutia chumvi mno, hadi kufikia kuvuka mstari wa uhalisia na mantiki. Kwa maneno mengine, fantasia ni dhana pana inayohusiana na chochote kinachoelezewa kwa kutiwa chumvi na kusimama nje ya uhalisia na mantiki. Uhalisia mazingaombwe ni aina fulani ya fantasia, lakini ni mbinu inayozileta dunia mbili pamoja za ‘ukale’ na ‘usasa’ –ukale wenye misingi ya mazingaombwe au ukweli ambao hauwezi kuelezeka katika mantiki ya nchi za Ulaya. Na usasa unaojaa taathira za kitamaduni, sayansi na teknolojia iliyoletwa na wakati wa ukoloni na wakati baada ya ukoloni. Tunaweza kusema kwamba Shaaban Robert ni mwanzilishi wa riwaya ya fantasia katika fasihi ya Kiswahili, hasa katika Kusadikika (1951), Adili na Nduguze (1952) na Kufikirika (1967). Lakini ingawa riwaya hizi zina uhalisia wa aina fulani, fantasia yake ni tofauti na ile ya riwaya mpya, kwa vile zimejikita mno katika ubunifudhanifu wa kila kipengele chake: ‘simulizi’, ‘hadithi’, ‘uhusika’, ‘mandhari’ na hata ‘uhalisia’ wa baadhi ya miketo7 ya matini yake. Fantasia ya riwaya mpya ni ya kuuelezea ukweli kama ulivyo hivi sasa na kwa hivyo uko karibu na kinachotokea katika mandhari, karibu na simulizi na wahusika wa riwaya yenyewe. Ingawa huu ni uhalisia mazingaombwe una mnato zaidi kuliko fantasia ya Shaaban Robert. Fantasia na uhalisia mazingaombwe ni pumzi za riwaya mpya. Huwezi kusoma ukurasa mmoja au hata pengine aya moja bila ya kujikuta unatoka katika uhalisia na kuingia katika mazingaombwe au kutoka mazingaombwe na kuingia katika uhalisia. Mpaka baina ya matukio au dunia hizi mbili ni mfinyu mno kiasi kwamba ni sawa na 7 Tafsiri ya Chunks kusema haupo. Mbinu hii imetawala katika riwaya zote za mwelekeo huu –mbinu ya uhalisia usio uhalisia, mazingaombwe yasiyo mazingaombwe, fantasia isiyo fantasia. Katika Nagona kuna mto unaonguruma usioonekana, ukohozi wa watu wasiokuwepo, miti inayocheka, hali ya mhusika kuchapwa na watu usiowaona, ukimya unaokatwa ghafla na sauti za watu wanaosoma wasioonekana (yote katika uk. 1 tu), maiti aliyefumbatwa katika kiza ambaye anashika Biblia mkono mmoja na Koran mkono mwingine, paka wa ajabu anayetarajiwa kuwa mlinzi wa mauti (uk.2-3), bustani yenye maua meupe yanayoteleza na kutoa mwangaza, maua na matunda ambayo hayawezekani kuvunwa (uk.13), kikundi cha wafu cha wanafalsafa mashuhuri, wanabiolojia, wanasosiolojia na wanasaikolojia wanaofufuka ... (uk.15). Katika Babu Alipofufuka kuna dhana nzima ya fikira kwamba hatufi, tunapita tu katika dunia nyingine ya kutoonekana tukiwa mizuka, dhana nzima ya ndoto anayoiota binadamu katika dunia yetu ya leo, ndoto ambamo ndani yake binadamu anajiona hana hakika kama yupo au hayupo, anaishi au amekufa. Pia katika riwaya hii kuna miujiza ya aliye hai kuweza kujiua na kujifufua tena au kujigeuza mchwa na kurejea tena katika umbo la kibinaadamu au kuzama chini ya ardhi na kuibuka baharini na tena ghafla kukanyaga nchi kavu. Katika Bina-Adamu kuna miujiza ya kutumika chakula na kinywaji kisichokwisha na ambacho kinashibisha mara moja. Au ya mhusika kuweza kusafiri dunia nzima kifikira au ndoto, kupitia nchi kavu na mtoni na baharini. Kuna hali ya mtu mzima kurudi utoto kimaumbile. Mna viumbe wa miujiza kama lile jitu lenye miguu mirefu kupita kiasi ambalo linaitwa beberu au UMERO-JAPA. Au aina ya kiumbe mwingine anayeitwa Wotan, Mungu wa vita na mfalme wa mashujaa. Au mahuntha watatu ambao wanatafutwa lakini hawaonekani kwa sababu ni viumbe wa miujiza. Kuna P.P (Peter Pan /Yanguis??) mwenyewe ambaye ana miujiza ya kinanga8 na kuzongwa na visaasili ambaye pia anatafutwa na mhusika mkuu ili iwe ni sababu ya kukikomboa kijiji kilichotengwa mno duniani. Viumbe wengine wa miujiza ni wale watu waliofufuliwa, akina Fyura (yaani Fuehrer, lakabu aliyopewa kiongozi wa kiimla Adolf Hitler), Dkt. Joseph Mengele, Hiro (Hirohito, aliyekuwa mfalme wa Japan), Osagyefo (yaani marehemu Kwame Nkrumah), Churchill na Stalin. Mwalimu au Mussa anayeishi vileleni mwa miti na ambaye anapenda sifa na kuimbiwa nyimbo (labda marehemu mwalimu Nyerere). Katika Ziraili na Zirani kuna mpaka mdogo sana wa maisha ya duniani na mbinguni. Kuna mchanganyiko wa watu, malaika na Uungu. Kuna roho kusimama na kusema au ufufuzi wa watu wanaosema na majini, mashetani na malaika. Pia katika riwaya hii maisha ya mbinguni yanachorwa kisitiari na kufananishwa na maisha yetu tuliyonayo leo: maisha yaliyojaa suitafahamu za kiitikadi za kidini na siasa, uonevu, mabavu, unyonyaji, uongo, unafiki, ufisadi, njama, ugomvi na vita. Mlinganisho huu ni wa uhusiano wa karibu mno mpaka msomaji anajiuliza kama mwandishi anazungumza kwa njia ya ishara na fumbo, ahera au dunia tunayoishi leo. Katika Dunia Yao, mazingaombwe yamo katika ile hali ya mhusika kuikimbia nafsi yake, familia yake, marafiki, majirani na jamii kwa jumla; ile hali ya mporomoko wake unaomrusha akili na kumfanya aishi kwenye chumba kidogo mfano wa jela ambamo anazurura katika dunia pana bila ya kuzurura. Anamozurura katika ndoto. Katika dunia hii mhusika mkuu anapanga udugu na kompyuta, mtu-mashine pekee 8 Tafsiri ya Epic aliyebaki katika maisha yake anayeweza kumwamini, kuzungumza naye, kushauriana naye, kumtumia kama kiwango cha kuandikia historia na hadithi yake na hadithi za watu wengine na kiwambo cha kuweza kuzungumza na binti yake ambaye anaishi London kama mkimbizi-njaa. Kuna wahusika-picha wanaosimama kutoka katika albamu na kuwa viumbe vyenye ngozi, nyama, damu na mifupa –viumbe vyenye urazini kamili. Ndani ya riwaya hii pia kuna mtoto mkombozi9 ambaye tokea siku yake ya kuja duniani anaonyesha miujiza ya kusema, kula, kutembea na kutoa rai kama vile mtu mzima. Pia katika riwaya hii kuna matambiko yanayohusishwa na Miungu ya Kiafrika kama ile ya kosmolojia ya Waibo wa Nigeria. Jambo muhimu hapa ni kukumbuka kwamba fantasia na uhalisia mazingaombwe hayapo kwa ajili ya kuwepo tu au kwa ajili ya mchezo wa lugha na sanaa. Ni mbinu muhimu ya kumfanya msomaji autupie jicho kali uhalisia mpya ambao una ukweli wa aina nyingine kabisa, uhalisia wenye mkanganyo na utata. Ni mbinu ya kukemea kile kinachoonekana na waandishi hawa kuwa ni utandawizi badala ya utandawazi. Ni mbinu ya kuonyesha mporomoko wa kila kitu katika jamii zetu –uchumi, utamaduni, uhusiano baina ya mtu na mtu, uhusiano wa raia, umakinifu wa ukoo na mtu binafsi kama Mtanzania na Mkenya, utambulisho wa mtu binafsi ambao umesambaratika na kuteremka chini kwa kiwango kikubwa mno, au kuporomoka kwa huduma za kijamii, kunajisika kwa heshima ya Mwafrika, Mtanzania, Mkenya na mpopote-pale-alipo ulimwenguni. Ushahidi mzuri wa fantasia na uhalisia mazingaombwe umo katika dondoo hili la Mohamed katika Dunia Yao (uk.172-173) – dondoo ambalo linaelezea dhana ya utandawazi katika picha za kimiujiza kabisa: Sasa hivi ndiyo kile kitu kimeshakaribia. Karibu mno kuweza kutambulikana. Kitu gani? Ilikuwa vigumu hata kubahatisha kukiagua au kukitaja kwa asahi. Kitu au jitu? Utata wa jitukitu labda. Umbo lake limekas’mika nusu bin nusu, kushoto na kulia, katikati ya jimwili lake. Pandikizi la jitukitu jinsi lilivyoumbika. Kushoto, linamemetuka anga la ki- Ungu linaloumiza macho na kuogofya. Kushoto pia linachanua uzuri wa ajabu. Uzuri wa kike ndani ya uzuri wa kiume. Uzuri unaokanganya. Sijapata kuona kiumbe duniani chenye uzuri namna hii. Useme hao huru-l-ayen wa peponi watajikanao. Na kulia, jimwili lake limekumbatiwa na giza zito la maangamizi ambalo kila mara lilikuwa likiripuka moto kuunguza kila kitu kilichosimama kwenye njia yake. Lilikuwa likipita kwa kasi ya umeme, lakini bado lilionekana lipo papo hapo daima – haliondoki! Linapiga kasi katika njia yake inayojiandika yenyewe – mara Globalization mara Americanization. Na lilipotimka lilitifua kila kitu katika kasi na mikiki yake. Kila kitu kilipojaribu kufukuzana nalo, kilijikuta kinaachwa nyuma milioni ya kilomita. Likapita kwa kasi na pepo zake za dhoruba likiripuka mandimi ya moto yaliyounguza na kukausha kila kitu: watu, wanyama, barabara, majumba, miji, maji, hewa, pwani, bahari, nchi kavu, madini, umeme, mafuta, hospitali, madawa, benki, viwanda, biashara, raslimali zote ... shule, vyuo, desturi, mila, tamaduni na hata uhai, heshima na mustakabali wa watu – hata roho zao. Lilipenya hata ndani ya nyumba na vibanda vya watu kusasambura na kupekua kila kitu kukashifu na kufedhehi na kisha kuangamiza lilivyopenda. Liliingia humo na kutawala na kuamrisha na kulazimisha mambo katika nyumba yake mwenyewe mtu ... Ingawa huu si mkemeo kamili (labda ni maombolezo), bado lakini tunaona hasira za mwandishi na kutokubaliana kwake na dhana ya utandawazi iliyoingia katika vichwa vya 9 Katika riwaya hii mpya ‘mkombozi’ ni neno muhimu sana linalorejelewa katika nyingi ya matini ya riwaya zenyewe viongozi na watu wetu. Ni dondoo linaloonyesha aina ya kuwezwa vibaya sana ukilinganisha na zile siasa za miaka ya 1960 hadi 1970 zilizotupa tamaa ya kukwamuka na kuwa na ufahari wa kuwa sisi ni watu pia. 3.4 Lugha ya Mchanganyondimi10 Gromov (2004:6) anapiga ndipo anaposema kwamba sifa moja muhimu ya riwaya hii mpya ya Kiswahili ni ile ya mchanganyondimi. Lakini Gromov haishii hapo, anafafanua mchanganyondimi kama unavyotumika katika riwaya hii kwa kuuita mchanganyondimi wa mbambizoviraka11. Kwa mfano, hadithi ya Babu Alipofufuka inaanza kama hadithi ya mzuka, kisha inaingia katika maelezo ya matukio ya uhalisia katika jiji mojawapo la nchi za Kiafrika na baadaye inamwongoza msomaji katika ukweli wa kifantasia ambao umo katika dunia nyingine. Tena tunaelezewa kuporomoka kwa Pate ya Al-ikishafi. Kisha inakuja habari ya UKIMWI ikifuatiwa na uharibifu wa tabaka ozoni. Halafu tunakutana na Visaasili vya Wagiriki na Mungu wao wa pwani, yaani Proteus ambaye anahusishwa na utandawizi wenyewe au kiongozi mkuu wa nchi za Kiafrika ambaye anautumikia utandawizi huku akienda dhidi ya nchi yake na watu wake. Wamitila katika Bina-Adamu, pia anatumia mchanganyondimi usio mipaka ya urejeleshi12 kuhusu ‘matokeo ya historia za dunia’, ‘fasihi’, mchanganyo wa ‘visaasili’, ‘matini za kidini’, ‘falsafa’ na mambo muhimu ya uhalisia wa maisha ya kisasa. Riwaya hii pia inaingiza wababe kama Wotan, Pandora, Joseph Mengele, Emperor Hirohito, Che Guevara na maandishi ya Heike Monogatari na William Dubois’ The Soul of Black Folk. Katika riwaya mbili za Kezilahabi, Nagona na Mzingile kuna mchanganyondimi wa aina hiyohiyo, ingawa kwa mtindo na nyenzo tofauti. Kwa mfano, matini inajengwa kwa lugha faragha ya mwandishi mwenyewe anayejificha nyuma ya wahusika wake, lugha ambayo imo katika mkondo simulizi, lakini kila mara inaingiliwa kati na miketo ya kifilosofia, dini, saikolojia, maneno ya mitume waliofufuka na wahusika wengine wenye uwezo wa kuishi maelfu ya miaka. Hivi ndivyo miketo hiyo inavyopachikwa kimbambizoviraka juu ya matini kuu ya riwaya ya Nagona (uk.15): Uwaonao katika duara hii ni kikundi kidogo tu cha waliokuwa wabishi katika usakaji wa njia. Yule pale ni Plato, na yule ni Socrates. Huyu hapa ni Aristotle. Yule ni Hegel huyu ni Darwin na waliokaribiana na Marx ni Freud na huyu ni Nietzsche ... Na si kama wafu hawa wanatajwa majina tu – lakini pia wanaonyeshwa kushiriki katika historia yao ya mapambano ya kifalfasa na kiitikadi kama pale tunapoambiwa: [S]asa hivi wametulia kidogo. Zamani wakianza majadiliano na roho zao ilikuwa vurugu tupu. Na wakianza majadiliano ya wao kwa wao basi hapo duara iliwaka moto ...(uk.15) 3.5 Lugha na Falsafa Kwa kawaida matukio makuu yote yanayokuja kuwaelemea watu vibaya sana, huzusha mijadala ya kifalsafa. Kuzuka kwa neno utandawazi na taathira ya neno hili katika maisha ya watu katika ubinafsi wao, ujamii wao, utamaduni wao, imani zao za kijadi na 10 Tunalitumia neno hili kwa maana ya ‘collage’, yaani mbandikizo wa picha mbalimbali ambazo si lazima ziwe na uhusiano wa moja kwa moja juu ya mji wa sanaa ya uandishi 11 Tunalitumia neno hili kwa maana ya ‘collage’, yaani mbandikizo wa picha mbalimbali ambazo si lazima ziwe na uhusiano wa moja kwa moja juu ya mji wa sanaa ya uandishi 12 Tafsiri ya Allusion kidini, kuwepo kwao duniani kiujumla, kuwepo kwao duniani kama kikundi cha watu wa jinsi fulani, kuangamia kwao, mwelekeo wao wa maisha ya baadaye, utambulisho wao, heshima yao kama binadamu ni mambo kadha ambayo bila ya shaka yanazua masuala ya kifalsafa kama vile: nini mtu? Nini utu? Nini ubinadamu? Nini uraia? Nini uzalendo? Nini ukweli na nini uwongo? Nini uhuru? Nini siasa? Ipi siasa bora? Nini historia? Nini dini? Kwa nini mtu alazimishwe kugeuza imani yake? Kwa nini mtu alazimishwe kuishi wanavyotaka watu wengine? Nini raha na furaha? Nini maendeleo? Haya ni baadhi ya masuala machache yanayoulizwa katika riwaya hii ambayo inaweza ikaitwa riwaya ya kisomi au kifalsafa. Kazi zote kwenye mkusanyiko wa riwaya hii, kwa namna fulani, zina kipengele hiki muhimu cha usomi ambamo falsafa ya aina fulani inajadiliwa na kuendelezwa au kuchokozwa. Nagona inajishughulisha mno na suala la kutafuta ukweli. Safari yote ya mhusika mkuu ‘mimi’ ni safari ya kuutafuta ukweli ambao unaonyeshwa katika riwaya hii una nyuso nyingi. Mzingile inakita katika mzugiko wa akili wa mwanadamu katika kuumba hofu kwa dhana (kwa mujibu wa mwandishi) yake mwenyewe – dhana ya Uungu – kwa hivyo suala la nini dini? Nani Mungu? Ni dhana gani ya Uungu? Ina dhima gani dini katika maendeleo ya mwanadamu? Ziraili na Zirani inasaili haki ya dini moja kujiona bora kuliko nyingine iwapo lengo hatimaye ni kumwabudu Mungu mmoja yuleyule. Kwa nini watu wanagombana na kupigana katika vita vikali vya jihadi ikiwa ukweli wa Uungu ni mmoja na dini hatimaye zinafanana sana? Aidha inalaumu uwezo wa Kiungu unaosababisha tofauti za kimaisha hapa duniani. Kwa nini wengine wamepewa nafasi ya kuishi bora zaidi kuliko wengine na Mungu wao ni yuleyule mmoja? Jambo hili limeleta kani ya kufanyika mapinduzi mbinguni yakiongozwa na waasi akina Zirani, mhusika mkuu na wenzake wengine wenye msimamo wa kimaendeleo. Katika Babu Alipofufuka, Dunia Yao na hata Bina-Adamu, suala zima linaloshughulikiwa kifalsafa ni siasa. Nini maana ya uongozi au uongozi bora? Nini uhuru? Nini maendeleo? Nini maana ya kuishi? Nini uraia wa mtu? Nini uzalendo? Kwa nini pesa ina nguvu zaidi kuliko kitu chochote –hata zaidi ya heshima ya mtu? Zaidi ya mke na mtoto wake mtu? Zaidi ya hata nafsi yake mtu? Kwa nini kikundi kidogo cha watu kipange maisha ya watu wengi katika jamii fulani na nje ya jamii hiyo? Kuna dunia ngapi katika dunia moja ya jamii fulani? Mipaka ya dunia hizo ni miembamba au mipana kiasi gani? Nini maana ya kifo? Nini maana ya kuishi? Inawezakana mtu ambaye anaishi kuwa ameshakufa? Nguvu zipi zinaongoza ulimwengu wetu? Zinaongoza kwa masilahi ya nani na kwa taathira gani? Katika Bina-Adamu (uk. 53) na riwaya nyingine nguvu hizi zinaelezewa kwa ungamo la nguvu zenyewe zinazojieleza hivi: [I]takuwa vigumu kupambana nami ... Nimewaingia akilini kabisa. Ninahisika kwingi hata nisikokuwako. Kutokuwako kwangu ndiko hasa kuwako kwangu! ... Mwandishi wa Bina-Adamu (uk.154-155) anafikia hata kupendekeza kwa maneno ya wazi wazi namna gani ya kupambana na nguvu hii: [J]amii inahitaji kuelimishwa upya kuanzia chini hadi juu, mtoto hadi mzee, wote ... e.e. Huu ndio ukombozi ufaao; matakwa ya jamii yawekwe mbele. Kumbuka siku za ukombozi kuletwa na mtu mmoja zimepita! ... Unganeni kiuchumi, kisiasa na kijamii. Umoja ni nguvu! Mtaishia kumfunga yeyote, awe mkubwa! Nilikumbuka kile kisa cha Gulliver; jitu kubwa lililoishia kufungwa na wale mbilikimo waliokuwa wakiitwa Lilliputians ... Kwa njia hii mtaacha kuishi pembezoni pembezoni mwa kijiji! Itabidi tuwe nguli kupambana na hasidi wa kijiji – Global villain. 3.6 Lugha na Mvunjiko wa Utambulisho Uharibifu mmoja mkubwa sana wa utandawazi au bora tuseme utandawizi ni ule wa nguvu zake za kuvunja na kuharibu utambulisho wa watu katika viwango mbalimbali: kibinafsi, kinchi au taifa, kisiasa, kiuchumi, kijamii, kiutamaduni na kidini. Tunaambiwa katika Bina-Adamu (148) ... [U]limwengu umekuwa kijiji kidogo siku hizi, mipaka haipo tena ... Mtu binafsi amevunjikavunjika kwa sababu hana pahala pa kusimama katika kudai haki zake za msingi kama vile kuweza kupata kazi ya kumwendeshea maisha yake kwa sababu utandawazi/utandawizi umevuka mipaka na kuvunja kuta kuchukua vyombo vya taifa na kuvitia katika mitaji na utajiri au masilahi yao: viwanda vimenunuliwa, benki zimechukuliwa, machimbo ya madini na rasilimali nyingine yamehodhiwa, vyombo vya huduma vya wananchi kama mashirika ya usambazaji umeme vimebinafisishwa, huduma za maji na mafuta na sehemu ya shule na hospitali hazimo tena mikononi mwa serikali za wananchi. Uko wapi usalama wa taifa ukizingatia haya? Kinchi au kitaifa utandawazi/utandawizi umevunja nguvu na uwezo wa maamuzi ya nchi kiuchumi na kijamii. Nchi na taifa lazima zifuate masharti ya vyombo vinavyotetea utandawazi kama vile WTO. Kwa maneno mengine nchi changa ambazo haziwezi kujitegemea, sio tu hazina tena sauti katika mambo ya kiuchumi bali pia katika yale ya kisiasa na ya kidunia. Ni ajabu, kwa mfano, kuona kwamba nchi za Kiafrika au Dunia ya Tatu hazina msimamo wa dhahiri wa suala la ujangili na vita vinavyoendeshwa Iraki na Afghanistan –kimya kimetawala katika nchi hizi ambazo miaka iliyopita zilikuwa mstari wa mbele kukemea matendo ya mataifa makubwa. Ni muhimu kuwa na msimamo wa mambo haya kwa sababu Waswahili husema ukimwona mwenzako ananyolewa na wewe tia maji. Sikwambii tena kiutamaduni, nchi changa zimekuwa nchi pokezi za tamaduni za wenzetu na hasa zile mbaya, hata maana ya utandawazi inageuka kuwa utanda-upande-mmoja. Katika riwaya hii mpya, lugha inayotumika mara nyingi ni ile ya kutokuwa na hakika tena ya jambo lolote. Hakuna hakika ya chakula, makazi, elimu, matibabu, heshima ya mtu, heshima ya nchi, uraia wake mtu, heshima ya Uafrika ambayo tokea mwanzo ilikuwa imekandamizwa sana wakati wa ukoloni. Mambo haya yote ndiyo yaliyokuwa msingi uliofanya nchi za Kiafrika na Dunia ya Tatu kupigania uhuru. Jambo hili limemfanya Wamitila kulalamika na kuhitimisha udhalimu wa utandawazi katika Bina-Adamu (uk.137) kwa kusema: [H]izi SAPS13 zinatusapa uhai ... Kijiji cha wizi hiki ... Dola inatukaba ... Yen ni kamba ya kitanzi! Ushahidi wa malalamiko haya umo pia katika Babu Alipofufuka (uk. 154) pale tunaposoma kwenye mabango ya maandamano ya kupinga utandawizi: ... M’mezifisidi nafsi zetu ... M’meivunja heshima yetu ... Vijana wetu wanapotea ... Vifo vya njaa na maradhi sababu si sisi ... Hatuna nafasi panapostahiki nafasi zetu ... Ardhi inachukuliwa hivihivi tunaona ... Kesho yetu imo katika giza ... Tunaangamia ... Tumeshakwenda kapa ... 13 Kwa urefu ni ‘Structural Adjustment Programmes’ Na hivi ndivyo tunavyomsikia mhusika mkuu Ndi-14 katika Dunia Yao (1) akilalama jinsi alivyovunjika kibinafsi... [L]abda nipo. Pengine sipo! Tofauti gani? Ndiyo, moyo bado unatuta. Hii labda ndiyo ishara pekee iliyobaki. Pangaboi linapepea pasi na nguvu za umeme. Kishumaa kidunya kinadiditia na kujitahidi kunilaza salama. Sijui lini lakini. Mwaka gani? Mwezi gani? Siku gani? Saa? ... Wakati hauwaziki tena –mashiko hauna, mantiki umeachana – umepoteza maana! Saa inatik’tika mezani. Inasonga mbele. Aaaa, saa! Chombo tu; na nambari zake, ishara ya jinsi wakati unavyokupuka –kasi, kasi; kasi isiyo kizuwizi. Lakini mbele nd’o wapi? Na nyuma ndiko kupi? N’navyojua mimi, wakati umeketi kichwani. Si juu ya uso wa saa ... 3.7 Mbinu Lugha zenye Mnasaba na Utandawazi/Utandawizi Kuna baadhi ya mbinu lugha ambazo waandishi wa riwaya hii wanazitumia kwa makusudi kuonyesha tabia na taathira ya utandawazi kwa nchi zetu. Mbinu ya kwanza ni ile ya maneno ambayo wameyaunda kuelezea hali hiyo. Kwa mfano, katika Babu Alipofufuka tunakuta meneno ‘uleo-wa-mawazo’, ‘ndoto-macho’, ‘kurongofywa’, ‘ukofiwatu’, ‘mkonowazi’, ‘mwambangoma’, ‘asijeurike’, ‘nakuona-wewe-mimihunioni’, ‘umaitikwenenda’, ‘mfuhai’, ‘watengeza-utamaduni-mpya’, ‘zizikinyesi’, ‘wenyesingazao’, ‘kizamoto’, ‘n’kupande-n’kushuke-kasheshe’, ‘tumejitoa-tumejitiawasasa’, ‘wapenda furaha’, ‘wapendakachiri’, ‘mmezakaseti’, ‘bwana-mwenye-nyumbakubwa’ n.k. Katika Dunia Yao tunasoma maneno kama vile: ‘pangaboi’, ‘mkaushausingizi’, ‘nyama- na- mifupa’, ‘kandamoyo’, ‘mtu- nyama– na- mifupa’, ‘baruapepe’, ‘wavumeme’, ‘umwamba- wa- kiume’, ‘kisichofaa- kinachofaa’, ‘babkubwa’, ‘elimujamii’, ‘wanaelimujamii’, ‘mkokota rikwama’, ‘dongo- la- zamani’, ‘mtapionuru’, ‘ki-TshombeTshombe’, ‘kimulatomulato’, ‘ki-hybridhybrid’, ‘ndoto-kweli’, ‘wauzatarabizuna- na- uzuri’, ‘Superboyswawili’ n.k. Katika Bina-Adamu, tunakutana na maneno kama ‘Bina-Adamu’, ‘wasichanawavulana’, ‘UMERO-JAPA’, ‘Zakongwe’, ‘Fyura’, ‘Fyuraha’, ‘rubo’, ‘Mefu’, ‘Yanguis’, ‘FUJO ASILIA’, ‘UMOJA WA FUJO’, ‘Jengo la Pembetano’, ‘zinatusapa’, ‘taifa-dola’, ‘Abubepar’, ‘Binberu’, ‘Mwajihawaa’, ‘Mwanakabila’, ‘Binrangi’, ‘Mkengeushi’ n.k. Pia riwaya hii inaingiza kwa makusudi maneno mengi ya kigeni kusisitiza usomi wa riwaya yenyewe na pia ugeni na wizi wa utandawazi wenyewe. Katika Nagona kwa mfano, tunapata maneno kama ‘Ego’, ‘Id’, ‘Superego’, ‘Sphinx’, ‘Cogito’, ‘Causa’ ‘Ultima’, ‘Disciplina Voluntatis’, ‘De Anima’, ‘Politica’, ‘Metaphysica’, ‘De Poetica’, ‘Totem’, ‘Oedipus Complex’, ‘Neurosis’, ‘ashab’, ‘tabilin’ na ‘tafsir’. Katika Babu Alipofufuka tunaona maneno kama ‘Gangar Wa’azu’, ‘Doggy’, ‘Neo- Casino’, ‘Proteus’, ‘Limonsin’, ‘shoyu’, ‘sake’, ‘beetles’, ‘spring chicken’, ‘semaa wa twaa’, ‘FKK’, ‘CD-ROM’, ‘Mona Lisa’, ‘zerha’, ‘manekineko’. Katika Dunia Yao tunapata maneno kama ‘Muse’, ‘CD’, ‘video’, ‘TV’, ‘taj’widi’, ‘maulidi’, ‘kasida’, ‘C Licence’, ‘TX’, ‘chip’, ‘Hillman’, ‘Vauxhall’, ‘mamluki’, ‘The Aritos’, ‘New World Order’, ‘WTO’, ‘Globalisation’, ‘sanctions’, ‘RAP’, ‘Paradise’, ‘I Need to Know’, ‘fantastic’, ‘Skyscrapers’, ‘cloning’, ‘dialectics’, ‘Zeus’, ‘Mnemosyne’, 14 Neno lenyewe kama jina la mhusika mkuu ‘Ndi-‘ limemeguka, limevunjika. ‘Calliope’, ‘Clio’, ‘Erat’o’, ‘Euterpe Melpomene’, ‘Polyhymnia’, ‘Terpsichore’, ‘Thalia’, ‘Urania’ n.k. Katika kipengele hiki pia tunaingiza uvunjaji wa kanuni za kisarufi, kiutanzu na kiujumi katika matini ya baadhi ya riwaya za mwelekeo huu. Uvunjaji huu unalinganishwa na uvunjaji wa kanuni kadha katika jamii ambazo zilidhaniwa zimeshakita na zisingeweza kuvunjwa kamwe. Ni wazi kwamba katika Babu Alipofufuka na Dunia Yao kanuni za sarufi zinavunjwa makusudi kama tunavyoona katika Babu Alipofufuka...[u]wanja-wa-ndege-wa-kimataifa alisimama kujitayarisha kwa ufunguzi wa milango (uk.29) ... komputa alimwambia kwamba mkewe Bi. Kiluba alikuwa akimsubiri kumbi la chini (uk.67). Au katika Bina-Adamu tunagundua kauli kama ...[I]nasemwa kuwa ... (uk.35) ambayo imechukuliwa moja kwa moja kutokana na Kiingereza balada ya Kiswahili Inasemekana kuwa ... [W]anaamini kwamba ukoo wao ni tukufu (uk.38) badala ya Ukoo wao ni mtukufu ... [H]apana, labda ni kimo changu cha mtoto (uk.45) badala ya Hapana, labda kimo changu cha utoto ... Matumizi wa sanaahati15 – yaani namna ya kucheza na mwandiko wa maneno ili kutoa hisia fulani ya kimaana au ujumi ni njia nyingine ya matumizi ya lugha kuelezea hali na taathira za utandawizi katika baadhi ya riwaya hizi, hasa katika Babu Alipofufuka, Dunia Yao na Bina-Adamu. Katika Babu Alipofufuka ukosefu wa uaminifu na kigeugeu cha utandawazi wenyewe na viongozi wakuu wa nchi wanaoutekeleza kwa shauku, unaelezewa katika mabadiliko ya uherufi katika sura mbalimbali kama vile tunavyoona katika neno Proteus linavyochorwa kiwimawima, kimlalo (kiyombo), kimkolezo, kimfifio, kiudogo na kiukubwa. Kwenye Dunia Yao tunapata nambari 36 ya miaka ya uhuru wa Zanzibar inakolezwa makusudi ili msomaji atafakari mafanikio na mashindikano ya wakati wa baada ya uhuru wa miaka hiyo 36. Maneno Wewe na mimi (uk.20) yanatofautishwa kwa mkozesho na udogowesho kusisitiza ubinafsi na ule ukilamtu- na-lake wa siku hizi. Usichochote nao unasisitizwa katika mpromoko wa maneno cider na nonentity. Neno Superboyswawili linalosisitiza Umarekani na Urusi wakati wa vita baridi linatiliwa mkazo na mkolezo wa wino. Neno ilhamu linalosisitiza kuzuka kwa riwaya mpya katika wakati wa utandawazi na kuwepo mtindo wa riwaya ndani ya riwaya (metafiction) au uzungumziaji wa riwaya ndani ya riwaya hasa kujibu hoja ya baadhi ya wahakiki kwamba riwaya sharti ichukue mkondo wa uhalisia – limekozeshwa wino pia. Bina-Adamu inatumia mkolezo wa wino au/na yombo na herufi kubwa katika msisitizo wa baadhi ya maneno yake kama Njia ya UHALISIA, UMERO-JAPA, Gastarbeiter, Nurenibaga, daktari wa kifo, Osagyefo n.k. Muhimu sana katika mbinu hii ni jinsi inavyotofautisha sauti za wasimulizi na wahusika mbalimbali katika riwaya ambamo herufi wima, herufi mlalo au yombo na herufi yombo zilizokolezwa, zinatafautisha wasimulizi na wahusika mbalimbali katika riwaya hii. Pia mbinu ya kuingiza mtindo wa utanzu mwingine katika utanzu wa riwaya kama vile tunavyoona Kezilahabi anapojenga matini yenye mtiririko wa kitamthilia (wa mazungumzo na majibu) katika sura 8 (uk. 47-52) yote inayojadili ufisadi, ngono na ukandamizaji wa kisiasa ulivyotawala duniani. Pia mwandishi huyu anavyotumia ufupisho wa sura yenyewe kama vile sura ya 10 (uk. 62) ambayo ina aya nne ndogondogo tu. Kwa kweli, riwaya za Kezilahabi ni fupi mno, kwa kiasi cha Nagona kuwa na kurasa 62 na Mzingile 70. 15 Tafsiri ya graphicart Mbinu ya mkarara wa kauli na maneno teuzi ni muhimu pia katika matumizi ya lugha –mbinu inayorejelea utandawazi/utandawizi na kusisitiza baadhi ya matokeo yake ambayo msomaji anatakiwa ayape uzito katika kuyafikiri. Katika Nagona maneno ‘ukweli’, ‘mshumaa’, ‘vichaa’, ‘vicheko’, ‘ungamo kuu’, ‘ukimya’, ‘njia’, ‘barabara’, ‘mto’, ‘paa’, ‘ndege’, ‘mti’, ‘msitu’, ‘milima’, ‘mabonde’, ‘duara’, ‘vitabu’, ‘ukosefu wa watu’, ‘paka’, ‘mkombozi’, ‘ajali’, ‘ndoto’, ‘maluweluwe’, ‘uta’ na ‘mshale’ ni maneno yanayorudiwarudiwa kila wakati. Katika Mzingile ‘mwanga’, ‘karne’, ‘kichaa’, ‘mkombozi’, ‘safari’, ‘ndoto’, ‘mto’, ‘giza’, ‘mzee’ na ‘ukungu’ ni baadhi ya maneno yanayorejewa kila baada ya muda. Katika Babu Alipofufuka maneno ‘Proteus’, ‘Limonsin’, ‘Doggy’, ‘mzuka’, ‘Neocasino’, ‘kimya’ na ‘kompyuta’ ni maneno yanayotajwa sana. Katika Bina-Adamu maneno ‘Bina-Adamu’, ‘P.P’, ‘huntha’, ‘Wotan’, ‘mto’, ‘safari’, ‘njia’, ‘Fyura’, ‘Yanguis’, ‘utandawazi’, ‘global village’ na ‘wizi’ ndiyo yanayojitokeza sana. Lakini mbali na neno moja moja, baadhi ya kauli au picha zinazojengwa kwa maneno mengi ambazo hurudiwa tena na tena kama tunavyoona katika Babu Alipofufuka (uk.92, 96) kauli ya La, hatutaki, hata ikiwaje hatulali tena... na katika Bina-Adamu (uk.140, 148) picha ya kuwa Ulimwengu umekuwa kijiji kidogo siku hizi, mipaka haipo tena ... inarudiwa tena na tena ingawa kwa maneno mengine. Kauli ya Hii ndiyo bustani yao ya Eden inarejewa mara kadha (uk.64, 110). Pia katika kitabu hikihiki tunakuta kauli Sio sisi tu akina Churchill, ukoo wa Kaiser, ukoo wa Gaulle, kina Franco na muhimu zaidi P.P. anafanya hivyo! Huu ni ulimwengu wa uwongo... (uk.50, 51). Picha nyingine zinazorudiwarudiwa katika riwaya hii ni ile ya hofu, ujinga, wizi, ufisadi, unanganyi na unyang’anywaji. 4.0 Hitimisho Mjadala tuliouendeleza katika makala haya unarejelea na kuthibitisha tasnifu maarufu katika somo la fasihi; ile tasnifu inayosisitiza kwamba, kama maisha ya mwanadamu mwenyewe, fasihi nayo lazima ibadilike hasa wakati wa matukio makuu ya kutisha au kufurahisha kama utandawazi/utandawizi ambayo yanabadilisha kwa kiasi kikubwa, maisha ya watu wa jamii fulani. Kwa sababu lugha ni nyenzo ya msingi ya kubunia na kuwasilishia kazi ya fasihi, basi lugha haina budi kukidhi kimaumbo, kimiundo na kikazi, mahitaji ya kazi ya fasihi na mahitaji ya jamii yenyewe inayobadilika. Marejeo Bertoncini, Elena. (2002): When Grandfather Came to Life Again – S. A. Mohamed’s New Novel Beyond Realism – makala iliyotolewa kwenye Kongamano la Kiswahili, Bayreuth. Dittemer, Clarissa. (2002/2003): Said Ahmed Mohameds “Babu Alipofufuka” ein magischrealistischer Roman – Kazi Maalum kwa Somo la Riwaya Mpya ya Kiswahili, Sehemu ya Fasihi za Kiafrika kwa Lugha za Kiafrika, Chuokikuu cha Bayreuth. Gromov, M. D. (1998). Nagona and Mzingile – Novel, tale or Parabole? Katika Jarida la ‘Afrikanische Arbeitspapiere 55: Kiswahili Forum V’, uk.73-78. ____________. (2004). Post-modernistic Elements in Recent Kiswahili Novels. Katika ‘The Nairobi Journal of Literature: The Journal of the Department of Literature, University of Nairobi’, 2, uk.28-36. International Labour Force and Information Group. 1998. An Alternative View of Globalisation, ILRIG, Cape Town. Jauch, Herbert (ed.). (2001). Playing the Globalisation Game: The Implications of Economic Liberalisation for Namibia, Labour Resource and Research Institute (LaRRI) Windhoek. Kezilahabi, E. (1990). Nagona. Dar-es-salaam University Press. ___________. (1990). Mzingile. Dar-es-salaam University Press. Khamis, Said A.M. 1999. Defamiliarisation and Experimentation in the Kiswahili Novel: A Case Study of Kezilahabi’s Novel: Nagona. Hotuba isiyochapishwa ya kupokea uprofesa Chuo Kikuu cha Bayreuth (Inaugural lecture). ________________. (2001). Fabulation and Politics of the 90s in Kezilahabi’s Nagona. Katika Toleo la ‘African Languages Literature in the Political Context of the 1990s’. Bayreuth African Studies 56 (2001): 119-133. ________________. (2003). Fragmentation, Orality and Magic Realism in Kezilahabi’s Novel: Nagona. Katika ‘Nordic Journal of African Studies’ 12(1), uk.78-91. King’ei, Kitula. (2002). Fantasy and Realism in the Modern Kiswahili Novel: A Critical Look at Babu Alipofufuka by Said A. Mohamed – an unpublished literary review. Mkangi, Katama. (1995). Walenisi. East African Educational Publishers: Nairobi. Mkufya, W.E. (1999). Ziraili na Zirani. Hekima Publishers: Dar-es-salaam. Mohamed, Said A. (2001). Babu Alipofufuka. Jomo Kenyatta Foundation: Nairobi. ______________. (2005). Dunia Y ao (kitatolewa na Oxford University Press: Nairobi). _____________. (2005/2006). Mkamandume (kitatolewa na Longhorn (K) Ltd: Nairobi). Murray, A. 2000. Public Sector Restructuring in Namibia – Commercialisation, Privatisation and Outsourcing: Implication for Organised Labour, LaRRI, Windhoek. Nicol Bran (ed.) (2002). Postmodernism and the Contemporary Novel: A Reader, Edinburgh University Press. Offiong, Daniel A. (2001). Globalisation: Post-Neodependency and Poverty in Africa, Fourth Dimension Publishing Co.: Enugu Nigeria. Rettová Alena. 2004. Afrophone Philosophies: Possibilities and Practice – The Reflexion of Philosophical Influences in Euphrase Kezilahabi’s Nagona and Mzingile. Katika Jarida la ‘Kiswahili Forum’ 11, uk. 45-68. Robert, Shaaban. (1951). Kusadikika. Nelson: London. _____________. (1967). Kufikirika. East African Literature Bureau: Nairobi. Ruigrok W & R van Tulder. 1995. The Logic of International Restructuring, Routledge: London/New York. Topan, Farouk, (2002). Babu Alipofufuka by Said A. Mohamed – an unpublished literary review. Wamitila, K.W. (1991). Nagona and Mzingile: Kezilahabi’s Metaphysics. Katika Jarida la Kiswahili 54 la (TUKI), Chuokikuu cha Dar-es-salaam, uk. 62-67. ____________. (1997). Contemptus Mundi and Carpe Diem Motifs in Kezilahabi’s Works. Katika Jarida la Kiswahili 60 la (TUKI), Chuokikuu cha Dar-es-salaam, uk. 15-24. ____________. (2002). Bina-Adamu. Phoenix Publishers, Nairobi.

No comments:

Post a Comment